Kikwete flags off joint EA military exercises
Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Jakaya Kikwete, ameyataka majeshi ya ulinzi katika nchi za Afrika Mashariki kuwa tayari kukabili tishio lolote la usalama na amani pamoja na kukabiliana na majanga katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
Rais Kikwete aliyasema hayo wakati akizindua zoezi la kijeshi la majeshi ya ulinzi kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki lililopewa jina la 'Mlima Kilimanjaro' likiwa na lengo la kuyajengea majeshi hayo uwezo wa kukabiliana na ugaidi na majanga mbalimbali.
Alisema zoezi hilo ambalo limefadhiliwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ni kielelezo kuwa nchi hizo zinaweza kuendesha shughuli zao hata bila kusubiri nchi wafadhili.
"Tunawapongeza wanajeshi wetu kwa kazi nzuri mnayofanya, lakini ningeomba kwa unyenyekevu muendeleze moyo huo kwa ajili ya amani, usalama na utulivu katika jumuiya yetu ya Afrika Mashariki," alisema.
Alisema wataalam wa mambo ya amani na usalama katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, wameshapanua mwelekeo wa shughuli za jeshi hadi kulinda amani, ukabilianaji wa majanga na kusaidia mamlaka za kiraia wakati wa matatizo.
Rais Kikwete alisema mabadiliko hayo yanaendana kabisa na mkataba unaounda Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao unaweka maslahi ya watu na usalama katika ajenda za mchakato wa kuunganisha nchi tano katika jumuiya hiyo.
“Zoezi hili kimsingi lina maana ya kuyawezesha majeshi yetu kuelewa kwa kina mtizamo wetu wa pamoja na pia kuyaanda kutekeleza majukumu yao vizuri wakati wa uhitaji," alisema.
Hata hivyo, alisema zoezi hilo la pamoja la kijeshi linazungumza kwa mapana juu ya ushirikiano na mahusiano mazuri waliyonayo nchi tano zinazounda jumuiya hiyo.
“Mahusiano miongoni mwa nchi zetu ni mazuri. Kuna imani na kujiamini miongoni mwa nchi zetu na hali hiyo ndiyo iliyowezesha zoezi hili la pamoja la kijeshi," alisema.
Rais Kikwete ana imani kuwa zoezi hilo likienda vizuri, litafungua ukurasa mpya kwa majeshi ya ulinzi na usalama katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kwani yatakuwa yanabadilishana utalaam, mbinu na medani za operesheni mbalimbali.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia shirikisho la kisiasa, Beatrice Kiraso, alisema jumuiya hiyo inakabiliwa na matishio mengi yakiwemo ya uzaagaji ovyo wa silaha ndongo ndogo na nyepesi na kukosekana kwa utulivu wa kisiasa katika nchi zinazoizunguka Jumuiya.
“Matishio hayo ni kama vile ya majanga ya asili na yale yanayosababishwa na matendo ya binadamu, umaskini, magonjwa, mipaka mirefu, uzaagaji wa silaha, migogoro ya ndani kwa ndani na ukosefu wa amani katika nchi zinazotuzunguka," alisema Kiraso.
Alisisitiza umuhimu wa jumuiya hiyo kujenga uwezo wake yenyewe ya kuweza kukabiliana na dharura yeyote itakayojitokeza inayohatarisha amani, usalama na utulivu.
“Tukiweza hilo tutakuwa tumejenga mazingira mazuri kwa uwekezaji na mendeleo katika eneo la Jumuiya yetu ya Afrika Mashari," alisema.
Zoezi hilo ambalo litafikia kikomo Septemba 23, mwaka huu na linawashirikisha takriban wanajeshi 1,600 wa kutoka katika nchi tano wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
|